UONGOZI
wa Simba SC umesema hauna imani na mabadiliko ya refa yaliyofanywa
kuelekea mpambano wao na Yanga SC Jumamosi na kwa sababu hiyo unakutana
katika kikao cha dharula haraka iwezekanavyo kujadili suala hilo,
ikibidi kususia mchezo huo.
Akizungumza
na MPIRA NA MAENDELEO jioni hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba
inayosimamia ushiriki wa timu katika mashindano pia, Zacharia Hans Poppe
amesema kwamba uongozi utakutana haraka kujadili mabadiliko hayo.
Kapteni
huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema taarifa
rasmi waliyokuwa nayo awali refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo ni
Israel Nkongo, lakini ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo
limemtaja refa tofauti, Martin Saanya.
“Haiwezekani
mabadiliko yafanyike ghafla, lazima kutakuwa kuna namna hapa.
Tunakutana mara moja kujadili na kuchukua hatua, ikiwezekana tunaweza
kugomea hiyo mechi, iwapo tutagundua kuna mchezo mchafu umeandaliwa
dhidi yetu,”alisema Hans Poppe.
Saanya
kutoka Morogoro ndiye ameteuliwa kuchezesha pambano la watani wa jadi,
Simba na Yanga SC la kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka nchini ili
kujionea nani zaidi baina ya miamba hiyo, Saanya atasaidiwa na Samuel
Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, wakati refa akiba
atakuwa ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Kamisaa
wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa
waamuzi atakuwa ni Leslie Liunda wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment